Alvaraz kuiongoza Hispania Kombe la Davis

HISPANIA: NYOTA wa tenisi duniani, Carlos Alcaraz, ataiongoza timu ya Hispania katika mashindano ya Kombe la Davis baada ya kikosi hicho kutangazwa na nahodha David Ferrer Jumatatu.
Alcaraz, ambaye ameshinda mataji saba ya Grand Slam, ataungana na Rafael Jodar, Alejandro Davidovich Fokina, Marcel Granollers na Pedro Martinez katika kikosi hicho kinacholenga kuipa Hispania taji la mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa kikosi hicho, Ferrer alisema anaamini Hispania ina timu yenye uwezo mkubwa, huku akieleza kufurahishwa na upatikanaji wa wachezaji wote aliowahitaji kwa ajili ya mashindano hayo.
Ferrer alisema Hispania ni miongoni mwa timu zinazotajwa kuwa na nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano hayo, akisisitiza kuwa ni jambo zuri kushiriki huku ikiwa na wachezaji wake bora.
Alcaraz, ambaye kwa sasa anashika nafasi ya tatu duniani, alikosa takribani miezi minne ya msimu kutokana na jeraha la kifundo cha mkono. Hata hivyo, alirejea katika mashindano ya US Open na baadaye kutwaa ubingwa wa Japan Open mjini Tokyo mapema mwezi Oktoba.
Hispania, ambayo ilimaliza ikiwa mshindi wa pili katika mashindano ya mwaka jana, itaanza kampeni yake kwa kucheza dhidi ya Austria katika hatua ya robo fainali. Endapo itasonga mbele, inaweza kukutana na Uingereza au Ujerumani katika hatua ya nusu fainali.
Mashindano ya Kombe la Davis yanatarajiwa kufanyika mjini Bologna, Italia, kuanzia Novemba 24 hadi 29, huku Hispania ikitarajia kutumia uzoefu na ubora wa kikosi chake kurejesha taji hilo baada ya kusubiri kwa miaka kadhaa.




