Athletics Kenya yasikitishwa na Jepchirchir

NAIROBI: SHIRIKISHO la riadha nchini Kenya (Athletics Kenya) limeeleza kusikitishwa na kusimamishwa kwa muda kwa mwanariadha nyota Peres Jepchirchir, baada ya kupatikana na majibu yanayoonesha uwepo wa dawa iliyopigwa marufuku iitwayo EPO.
Katika taarifa yake iliyotolewa Oktoba 26, 2026, shirikisho hilo lilisema linaendelea kusimamia misingi ya michezo safi na kuhakikisha wanariadha wote wanashindana katika mazingira yenye usawa.
Athletics Kenya ilieleza kuwa licha ya kusikitishwa na taarifa hiyo inayomhusu mwanariadha huyo mashuhuri, haitalegeza msimamo wake dhidi ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku katika michezo.
Shirikisho hilo pia lilieleza kuunga mkono kikamilifu juhudi za Kitengo cha Uadilifu katika Riadha (AIU) katika kupambana na matumizi ya dawa hizo, likisema taratibu zilizotumika katika upimaji na kusimamishwa kwa muda kwa Jepchirchir zilifanywa kwa mujibu wa kanuni za kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.
Kusimamishwa kwa Jepchirchir kulitangazwa Oktoba 23, 2026, baada ya AIU kueleza kuwa mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33 alipatikana na majibu chanya ya EPO katika sampuli iliyochukuliwa nje ya mashindano, kabla ya kushiriki na kushinda mbio za Sydney Marathon mwezi Agosti mwaka huu.
Jepchirchir ni miongoni mwa wanariadha mashuhuri wa Kenya waliokabiliwa na hatua zinazohusiana na ukiukaji wa kanuni za kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.
Awali, mwanariadha Kibiwott Kandie alipewa adhabu ya kutoshiriki mashindano kwa miaka saba baada ya kukataa kufanyiwa vipimo nje ya mashindano na kuzuia maafisa wa udhibiti wa matumizi ya dawa hizo kutekeleza majukumu yao.
Aidha, mwaka jana, mwanariadha Ruth Chepngetich, aliyekuwa akishikilia rekodi ya dunia, alisimamishwa kwa miaka mitatu baada ya kukiri kosa lililohusiana na kupatikana na dutu ya hydrochlorothiazide (HCZ).
Hata hivyo, kusimamishwa kwa muda kwa Jepchirchir hakumaanishi moja kwa moja kuwa amepatikana na hatia ya mwisho, kwani shauri lake linapaswa kufuata taratibu husika za kinidhamu.




