Afrika Magharibi

AFCA wamkalia kooni Eto’o wamtaka ajiuzulu

YOUNDE, Cameroon: MUUNGANO wa Vilabu Vichanga Nchini Cameroon (AFCA) wamemtaka Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo, Samuel Eto’o kujiuzulu kwa kinachodaiwa kubaini hati ya uraia pacha wa Eto’o.

AFCA wanadai kiongozi huyo mkuu wa FECAFOOT ana uraia wa Cameroon na Hispania, hivyo anakosa sifa za kuendelea kuketi kitini.

Marais zaidi ya 50 wa vilabu nchini humo, wameiandikia kuitaka Kamati ya Nidhamu ya FECAFOOT kumuamuru Eto’o abwage manyanga.

Desemba 2021, Eto’o aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro Cha kutwaa kiti hicho ambacho inaelezwa kilikuwa na madudu mengi yaliyosababisha mgawanyiko katika soka la miamba hiyo ya Afrika.

Hata hivyo, miaka yake miwili uongozini amekumbwa na mizozo kadhaa ikiwemo dhidi ya Waziri wa Michezo na Elimu ya Michezo wa nchi hiyo, Narcisse Kombi kwa kilichoelezwa kuingiliwa mamlaka yake ya urais wa FECAFOOT.

Kumekuwa na fikra mseto juu ya uwezo wa kuongoza kwa mfumania nyavu huyo wa zamani wa Chelsea, Real Madrid na Barcelona ambaye wengine wakiamini ni mponyaji Ila wengine wakisema ni mwenye majivuno.

Je, Eto’o ataweza kuvuka kiunzi hiki? Tufuatilie hapa hapa ndani ya SpotiLEO.

Back to top button