Anunobi asimulia kifo cha mwanawe

NIGERIA: MUIGIZAJI mkongwe wa Nigeria, Eucharia Anunobi amefunguka kwa mara nyingine kuhusu maumivu aliyopitia kuhusu kifo cha mwanawe mwenye umri wa miaka 15.
Akizungumza katika mahojiano kwenye podikasti ya ‘The Honest Bunch Podcast’, Anunobi alidai kuwa uzembe wa kitabibu ulihusika katika kifo cha mwanawe.
Kwa mujibu wa mwigizaji huyo, mwanawe ambaye alikuwa katika hali mbaya hospitalini alipaswa kuongezewa damu, lakini badala yake mwanafunzi wa udaktari alimtoa damu.
“Badala ya kumpa damu, mwanafunzi wa udaktari alimtoa damu. Nilitoa takribani pints tatu za damu kutoka kwa mwanangu,” alisimulia kwa huzuni.
Anunobi alisema mwanawe alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya ugonjwa wa seli mundu (Sickle Cell Disease) kabla ya kufariki dunia mwaka 2017.
Aliongeza kuwa kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kwake, kwani mbali na kupambana na ugonjwa wa mwanawe, pia alikuwa akibeba mzigo mkubwa wa kifedha na kihisia wa familia jambo linalomuumiza hadi leo kila anapokumbuka kifo cha mwanae.




