Africa

Fountain Gate kutinga bungeni

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameialika bungeni Aprili 13 timu ya wasichana ya mpira wa miguu ya Fountain Gate ilyotwaa ubingwa wa Afrika kwa Shule za Sekondari hivi karibuni Afrika Kusini.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema hayo leo Dar es Salaam leo wakati akiipokea rasmi timu hiyo huku akiongeza kuwa Wizara itatoa zawadi ya shilingi milioni 10 kwa mabingwa hao.

Sehemu ya wachezaji wa timu ya wasichana ya Fountain Gate.

“Nakumbuka mara ya mwisho mliniahidi kutwaa ubingwa wa CECAFA tulipokutana Chamazi katika mashindano ya ukanda wetu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, na kweli mkatwaa ubingwa huo, mara ya pili tulipokutana tarehe 31, Machi 2023 mkaniahidi kutwaa Ubingwa wa Bara zima la Afrika katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini na kweli mkatekeleza ahadi yenu,” amesema Balozi Pindi Chana.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Wallace Karia amesema zawadi ya Dolla laki 3 waliyopata mabingwa hao imelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya michezo katika shule hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Shule ya Fountain Gate Japhet Makau ameahidi kuendelea kuibua na kuendeleza vipaji vingi kupitia shule hiyo.

Fountain Gate imetwaa tuzo za mchezaji bora, mfungaji bora na golikipa bora katika mashindano hayo ya Afrika.

Related Articles

Back to top button