AFCON

Kenya, Uganda: AFCON 2027 kuimarisha umoja Afrika Mashariki

DAR ES SALAAM: WAWAKILISHI wa Kenya na Uganda wamesema maandalizi ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ni fursa ya kuimarisha umoja wa Afrika Mashariki na kuonesha uwezo wa nchi hizo tatu kushirikiana katika kuandaa tukio kubwa la kimataifa.

Wakizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wamesema mashindano hayo yatakuwa zaidi ya soka, kwani yatatoa nafasi ya kukuza utalii, biashara, utamaduni na mahusiano ya wananchi wa nchi hizo.

Waziri wa Michezo wa Uganda, Peter Ogwang, aliipongeza Tanzania kwa juhudi za kuandaa mashindano hayo, akisema hatua ya CAF kuzikutanisha nchi hizo ni sehemu ya kuimarisha misingi ya ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Ogwang amesema mashindano hayo yana umuhimu mkubwa katika kuendeleza urithi wa viongozi wa awali wa Afrika Mashariki, akimtaja Baba wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere, miongoni mwa viongozi waliokuwa na maono ya kuunganisha ukanda huo.

“Mafanikio ya mashindano hayo yanahitaji maandalizi yanayozingatia miundombinu na usalama, si katika michezo pekee, bali pia burudani na utalii ili wageni waweze kufurahia huduma zote watakazohitaji,”amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya Hussein Mohamed amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania na Uganda kuhakikisha AFCON 2027 inakuwa mashindano yenye mafanikio na kuvutia ufuatiliaji mkubwa duniani.

Amesema AFCON ni tukio la kimataifa lenye uwezo wa kuunganisha mashabiki wa soka na kuwapa wageni nafasi ya kutembelea nchi zaidi ya moja katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote tatu.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa sekta ya utalii na maandalizi ya mashindano hayo ni muhimu katika kuhakikisha wageni wanaofika kwa ajili ya soka wanapata sababu za kutembelea vivutio vingine na kurejea tena baada ya mashindano kumalizika.

Related Articles

Back to top button