Tennis

Rehema: Tunahitaji maandalizi zaidi kufika fainali

PRAGUE: TIMU ya Taifa ya tenisi kwa wenye ulemavui imesema inahitaji kushiriki mashindano mengi zaidi ya kimataifa na kufanya maandalizi ya mara kwa mara ili kuongeza ushindani na kufikia hatua ya fainali katika mashindano yajayo.

Akizungumza na Spotileo nahodha wa timu hiyo, Rehema Selemani, amesema licha ya Tanzania kuishia hatua ya nusu fainali ya wachezaji wawili katika mashindano ya Karviná Indoor Open yaliyofanyika Jamhuri ya Czech, ushiriki wao umekuwa mzuri na umewapa uzoefu muhimu wa kimataifa.

Rehema na mwenzake Pendo Zengo waliondolewa katika hatua hiyo na Katarzyna Berthome wa Poland na Laura Valero wa Hispania kwa seti 6-2, 7-6 (4), matokeo ambayo nahodha huyo amesema yamewaonesha maeneo wanayopaswa kuboresha ili kukabiliana na wapinzani wenye uzoefu mkubwa.

Amesema changamoto kubwa iliyochangia kushindwa kufika fainali ni kutopata mechi nyingi za kimataifa za kujipima kabla ya mashindano, pamoja na tofauti ndogo ya uzoefu katika pointi muhimu za mchezo.

“Tunahitaji kufanyia kazi zaidi huduma ya kuanzisha mchezo (serve), kurudi kwa haraka baada ya kupiga mpira na utulivu wa kiakili tunapokuwa kwenye mechi zenye presha. Haya ni mafunzo mazuri kwetu,” amesema Rehema.

Ameongeza kuwa mashindano hayo yamewapa nafasi ya kujifunza kasi ya mchezo kwenye viwanja vya ndani, mbinu mbalimbali za wapinzani na namna ya kushughulikia nyakati muhimu za mechi, akisisitiza kuwa Tanzania haiko mbali na nchi nyingine zenye uzoefu mkubwa katika mchezo huo.

Kwa mujibu wa Rehema, timu hiyo inaendelea na mashindano ya Prague Indoor Open yanayoanza leo, kabla ya kutarajia kushiriki mashindano mengine nchini Austria Januari 2027.

Related Articles

Back to top button