Mastaa

Ariana Grande kunogesha filamu mpya ya Focker-In-Law

MAREKANI: MWANAMUZIKI na mwigizaji maarufu wa Marekani, Ariana Grande, amejiunga na waigizaji wakubwa katika filamu mpya ya vichekesho ya ‘Focker-In-Law,’ inayorejesha mfululizo maarufu wa filamu za ‘Meet the Parents’ baada ya miaka 16 tangu kutolewa kwa filamu iliyotangulia.

Katika filamu hiyo, Grande anacheza nafasi ya Olivia Jones, mchumba wa Henry Focker, mtoto wa Greg Focker anayeigizwa na Ben Stiller. Ujio wake katika familia hiyo unaleta changamoto mpya za kimahusiano na vichekesho vinavyojengwa kati yake na baba mkwe wake mtarajiwa.

Grande ameungana na waigizaji maarufu wakiwemo Robert De Niro, Ben Stiller, Owen Wilson, Blythe Danner, Teri Polo na Beanie Feldstein. De Niro anarudia nafasi yake ya Jack Byrnes, huku Stiller akiendelea kuigiza kama Greg Focker, wahusika waliofanya mfululizo huo kuwa maarufu.

Akizungumza kuhusu kushiriki kwake katika filamu hiyo, Grande alisema alifurahishwa na nafasi aliyopewa baada ya kusoma mswada wa filamu hiyo uliotayarishwa na John Hamburg. Pia alieleza kuwa ilikuwa heshima kwake kufanya kazi pamoja na waigizaji aliowaheshimu kwa muda mrefu katika tasnia ya filamu.

Kwa upande wake, Ben Stiller amemsifu Grande kwa uwezo wake wa kuigiza, akieleza kuwa alikuwa na kipaji, bidii na uwezo wa kuifanya nafasi yake iwe ya kuvutia. Stiller pia amebainisha kuwa mhusika wa Grande analeta changamoto mpya katika maisha ya familia ya Focker.

Filamu hiyo imeandikwa na kuongozwa na John Hamburg na imepangwa kuanza kuoneshwa katika kumbi za sinema Novemba 25, 2026. Ni muendelezo wa filamu za ‘Meet the Parents’ iliyotoka mwaka 2000, ‘Meet the Fockers’ ya mwaka 2004 na ‘Little Fockers’ iliyotoka mwaka 2010.

Related Articles

Back to top button