Muziki

Mariah Carey atamba spotify kupitia wimbo wake wa Krismasi

MAREKANI: MWANAMUZIKI nyota wa Marekani, Mariah Carey, ameendelea kuthibitisha ubora wake katika tasnia ya muziki baada ya wimbo wake maarufu wa Krismasi, ‘All I Want for Christmas Is You’, kushika nafasi ya kwanza kwenye chati ya kila siku ya Spotify nchini Marekani.

Wimbo huo ulipanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza baada ya kukusanya jumla ya usikilizwaji 935,863 ndani ya siku moja, hatua iliyouweka mbele ya nyimbo nyingine zilizokuwa zikishindania nafasi za juu kwenye chati hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya AceShowbiz, mafanikio hayo yanaonesha namna wimbo huo ulivyoendelea kuvutia wasikilizaji licha ya kutolewa miaka mingi iliyopita. Wimbo huo ulitoka mwaka 1994 na umekuwa sehemu muhimu ya muziki unaopigwa wakati wa msimu wa sikukuu za Krismasi.

Kupanda kwa wimbo huo kwenye chati kunahusishwa na kuongezeka kwa matumizi ya nyimbo za Krismasi kadiri kipindi cha sikukuu kinavyokaribia, huku mashabiki wengi duniani wakirejea nyimbo walizozizoea katika kusherehekea msimu huo.

‘All I Want for Christmas Is You’ ni miongoni mwa nyimbo zilizofanikiwa zaidi katika historia ya muziki wa Krismasi, ikiwa imeendelea kuweka rekodi mbalimbali kwenye majukwaa ya muziki wa mtandaoni na chati za kimataifa tangu ilipotolewa.

Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha nafasi ya Carey katika tasnia ya muziki duniani, huku wimbo huo ukiendelea kuwa sehemu ya utambulisho wake kisanii na kumuingizia umaarufu kila msimu wa Krismasi.

Related Articles

Back to top button