Ligi Ya Wanawake

Ubamba ang’ara, Madrid CFF yapaa nne bora Hispania

MADRID: MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Hasnath Ubamba, ameendelea kung’ara katika soka la Hispania baada ya kufunga bao na kuisaidia timu yake ya Madrid CFF kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Costa Adeje Tenerife.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake Hispania (Liga F Moeve) uliochezwa jana, kwenye Uwanja wa Heliodoro Rodríguez López, Ubamba alikuwa miongoni mwa nyota walioipa Madrid CFF ushindi huo muhimu.

Ubamba alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 27 kwa kumalizia pasi ya Sakina Ouzraoui, akiipa timu yake uongozi wa bao 1-0. Bao hilo lilikuja baada ya wenyeji kubaki pungufu kufuatia Elba Vergés kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 14.

Madrid CFF iliendelea kutawala mchezo na kuongeza bao la pili dakika ya 45+1 kupitia Emilie Holt, kabla ya Inès Konan kufunga bao la tatu dakika ya 68 akimalizia pasi ya Ubamba aliyefanya kazi nzuri katika shambulizi hilo.

Mbali na kufunga bao, Ubamba alionesha kiwango bora kilichomfanya atangazwe mchezaji bora wa mchezo (MVP), akithibitisha mchango wake katika safu ya ushambuliaji ya Madrid CFF.

Ushindi huo umeiwezesha Madrid CFF kufikisha pointi 20 baada ya michezo 12 na kupanda hadi nafasi ya nne katika msimamo wa Liga F Moeve, ikiendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana na timu zinazowania nafasi za juu.

Related Articles

Back to top button