Africa

Kocha wa zamani Yanga ajiunga Richards Bay

JOHANNESBURG: KOCHA Msaidizi wa zamani wa Yanga, Simo Dladla, ametangaza kuondoka klabuni hapo na kujiunga na Richards Bay FC ya Afrika Kusini ambako amepewa nafasi ya kuwa kocha mkuu.

Dladla, ambaye aliwahi pia kukaimu nafasi ya kocha mkuu wa Yanga, amesema amefikia uamuzi huo baada ya klabu hiyo kuelekea katika mfumo mpya wa kiufundi chini ya benchi jipya la ufundi.

Katika ujumbe wake kwa viongozi wa Yanga, Dladla amesema anaamini ni muhimu kumpa kocha mkuu mpya na wasaidizi wake uhuru wa kutekeleza falsafa na mfumo wao wa ufundishaji.

“Kwa hiyo, nimekubali changamoto mpya ya kuwa kocha mkuu wa Richards Bay FC nyumbani Afrika Kusini,” amesema Dladla.

Ameishukuru Yanga kwa kumpa nafasi ya kuitumikia klabu hiyo kama kocha msaidizi wa kwanza na baadaye kukabidhiwa jukumu la kukaimu nafasi ya kocha mkuu, akieleza kuwa ilikuwa heshima na sehemu muhimu ya safari yake ya ukocha.

Pia amewashukuru viongozi wa klabu hiyo kwa ushirikiano, weledi na mapokezi mazuri aliyoyapata wakati wa kipindi chake jijini Dar es Salaam, akisema Yanga itaendelea kuwa sehemu maalumu moyoni mwake.

Amesema bado yupo tayari kuitumikia Yanga endapo klabu hiyo itahitaji huduma zake siku zijazo, huku akiitakia mafanikio katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button