Bruno Fernandes asitisha mazungumzo ya mkataba mpya Man United

MANCHESTER: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, ameweka pembeni mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na klabu hiyo, akisema kwa sasa si wakati sahihi wa kujadili mustakabali wake Old Trafford.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 32 ana mkataba unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akiwa tayari amekataa ofa ya pili ya kuongezewa mkataba.
Fernandes amesema licha ya klabu kuonesha nia ya kumbakisha, hali ya sasa ya Manchester United haimfanyi kuwa tayari kuanza mazungumzo mapya.
Akizungumza na Sky Sports, alisema amekuwa na nafasi kadhaa za kuondoka katika misimu iliyopita, lakini amekuwa akichagua kubaki Manchester United kwa sababu ya mapenzi yake kwa klabu hiyo.
Nyota huyo pia alikanusha madai kwamba anadai mshahara mkubwa zaidi, akifichua kuwa aliwahi kupata ofa ya kujiunga na Al-Hilal ya Saudi Arabia ambayo ingempa nafasi ya kupata fedha nyingi zaidi.
Hatua hiyo inakuja wakati Manchester United ikiendelea kupitia kipindi kigumu, baada ya kufungwa mabao 4-0 na Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Anfield Jumapili.
Kwa upande wa kiwango chake, Fernandes amekuwa na wakati mgumu msimu huu, akiwa amefanikiwa kufunga bao moja pekee na kutoa asisti moja tangu alipotengeneza hat-trick dhidi ya Ipswich mwezi Agosti.
Mustakabali wake sasa unazidi kuwa suala la mjadala mkubwa, huku mashabiki wa United wakisubiri kuona kama nahodha huyo ataendelea kusalia Old Trafford au ataamua kutafuta changamoto mpya.




