Mitindo

Jihan, Nawat kuanza ziara Nigeria

DAR ES SALAAM: MSHINDI wa taji la Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, anatarajia kutembelea Nigeria kuanzia Novemba 18 hadi 22 mwaka huu, akiwa ameambatana na Rais wa mashindano hayo, Nawat Itsaragrisil, katika kampeni maalumu ya Ijue Lagos 2026.

Ziara hiyo imeandaliwa na Balozi Tomi Salami, Rais wa Aurora International Charity Foundation (AICF), ikiwa na malengo ya kutangaza utalii, kuimarisha mahusiano ya kitamaduni na kuwezesha vijana kupitia shughuli mbalimbali za kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Nigeria, kampeni hiyo itajumuisha mpango wa Inspire Africa Education & Empowerment Initiative unaolenga kuwafikia vijana 5,000 wa Lagos kupitia programu za ushauri, msaada wa elimu, vifaa vya usafi na shughuli za kuwawezesha.

Katika ziara hiyo, Jihan na Nawat pia wanatarajiwa kushiriki mapokezi maalumu, mkutano na waandishi wa habari wa kimataifa, ziara za heshima kwa viongozi na watu mashuhuri, pamoja na kutembelea maeneo ya urithi wa kihistoria ya Lagos.

Shughuli nyingine zitahusisha kuonesha mitindo ya mavazi na ubunifu wa Nigeria, ikiwa ni sehemu ya kutangaza utamaduni na vipaji vya nchi hiyo kimataifa.

Jihan, ambaye alitwaa taji la Miss Grand International Oktoba 10, 2026, jijini Bangkok, Thailand, aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushinda taji hilo tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button