Mastaa

Steph Curry amtetea mkewe kuhusu tukio la busu

MAREKANI: NYOTA wa mpira wa kikapu wa Golden State Warriors, Steph Curry, amemtetea mkewe Ayesha Curry kufuatia ukosoaji ulioibuka mitandaoni baada ya kuonekana akimbusu mwigizaji mwenzake, Matthew Daddario, katika filamu ya Krismasi ya ‘Second Chance Christmas’.

Curry, ambaye amekuwa kwenye ndoa na Ayesha kwa miaka 15, alijibu wakosoaji kupitia ukurasa wake wa Instagram Novemba 11, akisema baadhi ya watu wanajaribu kudharau mafanikio ya mkewe kwa kutoa maoni kuhusu maisha yao ya ndoa bila kuielewa kazi ya uigizaji.

Mshindi huyo wa mataji ya NBA aliwakosoa wachezaji wa zamani wa Warriors, Nick Young na Gilbert Arenas, waliomzungumzia Ayesha katika kipindi chao cha podcast ‘We Said What We Said’, huku wakimlinganisha na Savannah James, mke wa nyota LeBron James.

Pia aliwakosoa wachezaji wa zamani wa NFL, Emmanuel Acho na LeSean McCoy, ambao walijiuliza iwapo Ayesha alikubali nafasi hiyo ya filamu kwa lengo la kuvutia zaidi hisia za mumewe.

Steph alisema ukosoaji huo unaonesha namna baadhi ya watu wanavyoweka mipaka kwa wanawake kuhusu wanachopaswa kufanya.

Kwa upande wake, Ayesha alijibu mjadala huo kupitia mtandao wa X, akisisitiza kuwa tukio la kumbusu Daddario lilikuwa sehemu ya maigizo na si jambo halisi. Steph aliwataka wakosoaji kuomba radhi badala ya kuendelea kutoa maoni yasiyo na msingi.

Baada ya kauli hiyo, Nick Young aliomba radhi kwa Steph kupitia kipindi cha Gil’s Arena, akisema anampenda na kumheshimu. Hata hivyo, Arenas alitetea maoni yake ya awali, akisisitiza kuwa hakukusudia kumdhalilisha Ayesha bali alitaka kuonesha namna anavyomwona Steph kama mtu mwenye mwenendo mzuri katika maisha yake ya ndoa.

Related Articles

Back to top button