Summellah ataka lebo itakayompa nafasi sio kumweka benchi

DAR ES SALAAM: MSANII chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva, Nasra Abubakar maarufu kama Summerellah, amesema anatamani kusaini mkataba na lebo kubwa ya muziki itakayompa nafasi ya kufanya kazi na kukuza kipaji chake, badala ya kujiunga na kampuni itakayomuweka benchi kwa muda mrefu bila kumpa fursa ya kuonyesha uwezo wake.
Summerellah, ambaye ni mshindi wa nafasi ya tatu katika shindano la Bongo Star Search (BSS) 2026, amesema anaamini kuwa ana kipaji na uwezo wa kufanya vizuri katika tasnia ya muziki, hivyo anahitaji lebo itakayokuwa tayari kuwekeza katika kazi zake na kumpa ushirikiano wa kweli.
Akizungumza na SpotiLeo kuhusu mipango yake ya kimuziki, amesema ndoto yake ni kufanya kazi chini ya lebo yenye mipango ya kukuza wasanii wake, ikiwamo kuwapa nafasi ya kurekodi nyimbo, kuzitangaza na kuwafikisha katika viwango vya juu vya ushindani.
Amesisitiza kuwa hataki kusaini mkataba kwa sababu tu ya kutaka kuwa chini ya lebo kubwa, bali anahitaji ushirikiano utakaomuwezesha kuendelea kufanya muziki na kujenga jina lake.
Kwa upande wa wasanii anaotamani kushirikiana nao katika kazi zake, Summerellah ametaja majina makubwa ya Bongo Fleva akiwamo Ali Kiba, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, Marioo, Mbosso na D Voice kwa upande wa wanaume.
Kwa upande wa wasanii wa kike, ametaja Faustina Mfinanga maarufu Nandy na Zuhura Othuman ‘Zuchu’ kuwa miongoni mwa wasanii anaotamani kufanya nao kazi.
Amesema ushirikiano na wasanii hao utakuwa fursa muhimu kwake kujifunza, kubadilishana uzoefu na kupanua wigo wa mashabiki wake ndani na nje ya Tanzania.
Summerellah anaonekana kuwa na matarajio makubwa katika safari yake ya muziki baada ya kufanya vizuri katika BSS 2026, ambapo sasa analenga kutumia fursa alizozipata kupitia shindano hilo kujijenga na kuimarisha nafasi yake katika soko la Bongo Fleva.




