Afrika Mashariki

Maseneta watilia shaka Uwanja wa Kasarani kuelekea AFCON 2027

NAIROBI: KAMATI ya Bunge la Seneti la Kenya inayoshughulikia Masuala ya Kazi na Ustawi wa Jamii imeibua wasiwasi kuhusu utayari wa Uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani, kuandaa michezo ya AFCON 2027, kufuatia ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati wake kabla ya kukabidhiwa Desemba 31, 2026.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa West Pokot, Julius Murgor, imehoji kasi ya ujenzi, upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu na mifumo ya kukabiliana na dharura.

Seneta aliyeteuliwa, Crystal Asige, amesisitiza umuhimu wa kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, huku Seneta wa Kajiado, Seki Lenku, akieleza wasiwasi kuhusu usalama wa moto baada ya kubainika kuwa mabomba ya kuzimia moto hayakuwa na maji katika ukaguzi uliopita.

Hata hivyo, timu ya mradi inayoongozwa na Meja Daniel Makana imewahakikishia maseneta kuwa ukarabati unaendelea na uwanja utakamilika kwa wakati. Kasarani una uwezo wa kuchukua watazamaji 48,000 na ni miongoni mwa viwanja vitakavyotumiwa na Kenya katika AFCON 2027, pamoja na Talanta Sports City chenye uwezo wa watu 60,000.

Kenya itaandaa mashindano hayo kwa kushirikiana na Tanzania na Uganda. Hata hivyo, CAF inaendelea kutathmini maandalizi ya wenyeji hao baada ya ukaguzi wa Februari 2026 kubaini kuwa hakuna uwanja uliopendekezwa uliokidhi kikamilifu viwango vya Category 4.

Viwango hivyo vinahusisha ubora wa nyasi, taa, vyumba vya wachezaji, usalama, huduma za habari na miundombinu ya watazamaji.

Related Articles

Back to top button