Mwaikenda ataka Azam kudumisha makali

DAR ES SALAAM: BEKI wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda, amesema wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kuendeleza kiwango walichoonesha baada ya kuichapa Mbeya City mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mwaikenda amesema kila mchezaji aliyepata nafasi ya kucheza alijituma kwa kadiri ya uwezo wake ili kutimiza malengo ya benchi la ufundi, jambo lililoiwezesha timu hiyo kupata ushindi na pointi tatu muhimu.
Amesema licha ya kutoka katika mchezo mkubwa uliopita, wachezaji waliingia uwanjani wakiwa na dhamira ya kupambana na kutumia nafasi walizopata ili kupata matokeo mazuri.
“Naamini kila mchezaji aliyepata nafasi katika mchezo huu ametimiza wajibu wake na kuonesha imani ambayo kocha amempa. Kila mmoja amejituma kwa kadiri ya uwezo wake na hatimaye tumefanikiwa kupata mabao manne na pointi tatu,” amesema Mwaikenda.
Amesema malengo waliyojiwekea tangu mwanzoni mwa msimu, kwa kushirikiana na uongozi wa klabu, yanawataka wachezaji kutimiza majukumu yao katika kila mchezo ili kufikia matarajio ya timu.
Akizungumzia mashabiki, Mwaikenda amewashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono timu hiyo hata katika nyakati ngumu, akisema wachezaji wana wajibu wa kuwalipa kwa matokeo mazuri na kiwango kinachowafurahisha.
Ameahidi kuwa wachezaji wataendelea kujituma katika michezo ijayo ili kuipa Azam FC matokeo mazuri na kuwapa furaha mashabiki wake.




