Caf yarejesha mfumo wa awali wa Afcon

CAIRO: SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limefikia uamuzi wa pamoja kwamba Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) litarudi kufanyika kila baada ya miaka miwili.
Uamuzi huo umefikiwa kwa kauli moja na Kamati ya Utendaji ya CAF (EXCO), na kurejesha utaratibu uliokuwa ukitumika kabla ya pendekezo la kubadilisha michuano hiyo kwamba ifanyike kila baada ya miaka minne.
Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, alitangaza katika Mkutano wa Mkakati wa CAF uliofanyika Cabo Verde Oktoba 7 hadi 9, mwaka huu, kuwa kamati itafanya tathmini na mapitio ya uamuzi wa Afcon ifanyike kila baada ya miaka minne.
CAF imesema miongoni mwa sababu za kubadili msimamo huo ni kwamba mashindano mapya yaliyopendekezwa, Africa Nations League, yatahitaji miaka kadhaa kabla ya kuanza kuzalisha mapato makubwa yatakayogharamia mashindano ya CAF na kusaidia kukuza ushindani wa soka la Afrika kimataifa.
“Uamuzi wa kamati ni kwamba michuano ya Afcon iendelee kufanyika kila baada ya miaka miwili ulilenga kuendeleza, kulinda na kukuza maslahi ya soka la Afrika na vyama 54 wanachama wa CAF, pamoja na maslahi ya wachezaji wa Kiafrika wanaochezea klabu za nje ya Afrika.
“Tulikuwa na wasiwasi kuhusu muda mrefu unaohitajika kabla ya mashindano mapya yaliyopendekezwa ya Africa Nations League, kuweza kutoa mchango mkubwa wa kifedha na maendeleo ya soka, ili soka la Afrika na mashindano ya CAF yaweze kushindana katika ngazi ya kimataifa na kujitegemea kifedha,” alifafanua Dkt. Motsepe.




