50 Cent anataka Dola milioni 6 kwa Tia Kemp

CALIFORNIA: RAPA 50 Cent amefungua kesi dhidi ya Tia Kemp, kukomesha kile anachokitaja kuwa ni kumtumia mwanawe, Sire Jackson kama kifaa cha maonesho na chanzo cha mzaha.
50 Cent amefungua kesi hiyo kwa niaba ya Sire, 14 dhidi ya Kemp aliyewahi kuwa mpenzi wa rapa Rick Ross ambapo walijaaliwa mtoto wa kiume mwenye miaka 21.
Sakata la mzaha kwa Sire, lilianza punde baada ya 50 kutania kuhusu matukio mbalimbali ya kushambuliwa kwa familia ya Kemp.
Tangu wakati huo, Kemp amemshambulia hadharani 50 Cent na familia yake, ikiwemo Sire ambaye bado hajafikisha umri wa utu uzima.
“Bi. Kemp alitumia bila aibu maneno yanayohusu ‘wigo wa usonji’ kama tusi la kumdhalilisha mtoto, kwa lengo la kumvunjia heshima yeye na familia yake,” mawakili wa 50 Cent walieleza katika malalamiko yaliyowasilishwa mahakamani Oktoba 26, mwaka huu.
“Lakini usonji si jambo la aibu. Kinachotia aibu ni kubuni utambuzi wa kiafya kwa mtoto, kutunga sababu ya kudhalilisha kijinsia kuhusiana na hali hiyo, na kueneza mambo hayo kwa umma ili kumdhalilisha. Watoto na watu wazima wenye usonji wanastahili heshima na staha; usonji haupaswi kamwe kuwa kitu cha kudhihakiwa au kutumiwa kama silaha dhidi ya mtu yeyote, hasa mtoto.”
Rapa huyo, anaiomba mahakama kumuwajibisha Kemp kwa kusambaza kauli hizo ambazo alijua ni za uongo.
Pia, anaiomba mahakama itoe amri ya kulipwa fidia ya Dola milioni 6, imzuie Kemp kuendelea kutoa kauli kama hizo, na kuhakikisha kuwa mtoto huyo anapata ulinzi ambao sheria inamwahidi.




