Aziz Ki: Tutapambana kufika mbali Afrika

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Yanga, Stephane Aziz Ki, amesema timu hiyo itakabiliana na kila mchezo kwa umakini katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikilenga kufuzu hatua inayofuata na kwenda mbali zaidi katika mashindano hayo.
Yanga imepangwa Kundi B pamoja na Zamalek ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia, ikiwa ni kundi linalohitaji maandalizi na ushindani mkubwa kwa timu zote zinazowania nafasi ya kusonga mbele.
Aziz Ki amesema kikosi hicho hakitaki kujikita katika matokeo yaliyopita, badala yake kitaangalia kila mchezo kwa wakati wake huku kila mchezaji akijituma kusaidia timu kupata matokeo yanayohitajika.
Amesema lengo la Yanga si kushiriki tu mashindano hayo, bali ni kuvuka hatua ya makundi na kuendelea kupambana katika hatua zinazofuata.
“Jambo muhimu kwangu ni kucheza dhidi ya timu za aina hii na kusaidia timu yangu kupata ushindi. Lengo letu ni kuvuka hatua ya makundi kwa sababu tunataka kwenda mbali katika mashindano haya. Tutakachokutana nacho mbele yetu, tutajituma kwa nguvu zetu zote ili kufanikisha hilo,” amesema Aziz Ki.
Aidha, kiungo huyo amewashukuru mashabiki wa Yanga kwa kuendelea kuiunga mkono timu hiyo, akisema wachezaji wanatambua wajibu wao wa kufanya kazi kwa bidii ili kurejesha furaha kwa mashabiki.
Amesema hata wachezaji wenyewe hawafurahishwi na hali ambayo timu imekuwa ikipitia, akisisitiza kuwa wanapaswa kuongeza juhudi na kujituma zaidi ili kufikia matarajio ya klabu.
Aziz Ki amewaahidi mashabiki kuwa kupitia kazi ngumu na sapoti yao inayoendelea, Yanga itapambana kurejesha furaha na kurejea kwenye nafasi ya juu.




