2Face kukiwasha 30 ya Bongo Fleva

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI kutoka Nigeria, Innocent Ujah Idibia, maarufu 2Face, anatarajiwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaonogesha Tamasha la Miaka 30 ya Muziki wa Bongo Fleva litakalofanyika Novemba 7, 2026, jijini Mbeya.
Ushiriki wa 2face, ambaye ni miongoni mwa majina makubwa katika muziki wa Afrika, unatarajiwa kuongeza mvuto wa tamasha hilo linaloendelea kuwakutanisha wasanii wa ndani na wadau wa muziki katika kuadhimisha safari ya Bongo Fleva kwa miongo mitatu.
Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye akaunti ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Bongo Fleva, idadi ya wasanii wanaotarajiwa kushiriki tamasha hilo imeendelea kuongezeka kuelekea hatua ya Mbeya, huku mashabiki wakisubiri burudani itakayoambatana na maadhimisho hayo.
Maadhimisho hayo yalianza Julai 10, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kabla ya kuendelea Mwanza Agosti 8, Dodoma Agosti 22, Arusha Septemba 19 na Zanzibar Oktoba 17, mwaka huu.
Tamasha la Mbeya ni sehemu ya mfululizo wa matukio yaliyolenga kuenzi safari ya Bongo Fleva, muziki ambao umekua na kubadilika kwa miaka 30, ukitoa nafasi kwa wasanii wa vizazi tofauti kuonyesha vipaji vyao na kujenga taswira ya muziki wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Mbali na burudani, maadhimisho hayo yanalenga kutambua mchango wa wasanii walioasisi na kuendeleza Bongo Fleva, kuhifadhi historia ya muziki huo na kuwakutanisha wasanii, wadau pamoja na mashabiki wa muziki.
Kushiriki kwa 2face kunatarajiwa kuongeza uzito wa tamasha hilo la Mbeya, kutokana na nafasi yake katika muziki wa Nigeria na Afrika kwa ujumla, huku maadhimisho hayo yakiendelea kuwa jukwaa la kuangazia mafanikio yaliyopatikana na mwelekeo wa Bongo Fleva katika miaka ijayo.




