Mwandemele atwaa dhahabu Zimbabwe

DAR ES SALAAM: MTUNISHA misuli wa kimataifa kutoka Tanzania, Abraham Mwandemele, maarufu kama Alphathebeast, ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Harare Classic Fitness and Bodybuilding yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, nchini Zimbabwe.
Ushindi huo umeiwezesha Tanzania kupata mafanikio katika mashindano hayo yaliyowakutanisha wanamichezo kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa Mwandemele, hiyo ni mara ya pili kupata ushindi katika mashindano ya kimataifa baada ya awali kutwaa ubingwa wa Mr. East Africa BodyFuel yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Mafanikio hayo yanaendelea kuipa Tanzania heshima katika mchezo wa kutunisha misuli, huku yakionesha uwezo wa wanamichezo wa Kitanzania kushindana na kufanya vizuri katika majukwaa ya kimataifa.
Ushindi huo pia ni chachu kwa wanamichezo wengine nchini kuendelea kufanya mazoezi na kushiriki mashindano ya kimataifa ili kuinua kiwango cha mchezo huo na kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake.



