Muziki

Abigail Chams aweka rekodi Apple Music Tanzania

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Abigail Chamungwana, maarufu kama Abby Chams, ameweka historia kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike mwaka huu kushika nafasi ya kwanza kwenye chati za Apple Music Tanzania kupitia wimbo wake Me Too.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Abby Chams ameonesha furaha yake kwa mafanikio hayo kwa kuandika:

“Kutoka kwa msichana anayeishi kwa ajili ya muziki, hii ni ndoto kuwa kweli kwangu! Ningependa kuwashukuru nyote mnaoshiriki kwa ukaribu katika safari yangu. ‘Me Too’ ni wimbo mkubwa zaidi nchini kwangu kwenye majukwaa yote!”

Msanii huyo pia alimshukuru Harmonize, aliyeshirikiana naye kwenye wimbo huo, pamoja na mashabiki, familia, na timu nzima iliyofanikisha kazi hiyo.

Katika sekta ya muziki wa Bongo Fleva, ambayo mara nyingi inatawaliwa na wasanii wa kiume kwenye chati kubwa kama Apple Music, mafanikio ya Me Too yanaonesha nguvu na ushawishi wa Abby Chams katika tasnia hiyo.

Mashabiki na wadau mbalimbali wameendelea kumpa pongezi, wakisema huu ni mwanzo mzuri kwa wasanii wa kike kupenya zaidi kwenye soko la kimataifa.

Kwa mafanikio haya, Abigail Chams anazidi kuthibitisha kuwa ni sauti ya kizazi kipya cha muziki wa Bongo Fleva, huku Me Too ikionekana kuwa mlango wa kumfungulia fursa zaidi nje ya mipaka ya Tanzania.

Related Articles

Back to top button