Azam FC, Mbeya City kuumana leo

DAR ES SALAAM: AZAM FC leo inashuka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kuvaana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikilenga kupata pointi tatu zitakazoifanya kuimarisha nafasi yake katika msimamo wa ligi.
Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 17 baada ya mechi nane, huku Mbeya City ikiwa nafasi ya tisa na pointi 10 katika idadi sawa ya mechi, hali inayofanya mchezo huo kuwa muhimu kwa timu zote katika kutimiza malengo yao ya msimu huu.
Kocha wa Azam, Florent Ibenge, amesisitiza umuhimu wa wachezaji wake kutumia uwezo wa kiufundi, mbinu na nguvu kuhakikisha wanaibuka na ushindi, akionya kuwa hawapaswi kuidharau Mbeya City kwa kuwa nayo inahitaji matokeo mazuri.
Azam inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuiondoa ZED FC ya Misri katika Kombe la Shirikisho Afrika, ushindi ambao unaweza kuwa chachu kwa kikosi hicho kurejea katika ushindani wa ligi ya nyumbani.
Kwa upande wa Mbeya City, inahitaji kuboresha matokeo yake baada ya kupoteza mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar na JKT Tanzania, hivyo mchezo wa leo utakuwa nafasi ya kujaribu kurejea kwenye ushindani na kujiongezea pointi.
Rekodi ya timu hizo inaonesha kuwa mchezo unaweza kuwa na ushindani, baada ya kutoka sare ya bila kufungana walipokutana Aprili mwaka huu.
Mchezo mwingine utakuwa ni Coastal Union dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa saa 3:00 usikum kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Coastal Union inaingia kwenye mchezo huo baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Namungo matokeo ambayo yanaifanya ihitaji kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani ili kurejea kwenye ushindi.
Hata hivyo, Kagera Sugar nayo inahitaji matokeo mazuri baada ya kufungwa bao 1-0 na JKT Tanzania katika mchezo wake uliopita. Kabla ya hapo, ilitoka sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania, hivyo itakuwa na jukumu la kuboresha umaliziaji na uimara wake katika mchezo wa leo.



