Mastaa

Lulu: Ndoa nzuri ni ya ridhaa sio kulazimishana 

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Lulu Elizabeth Michael, amesema anaamini ndoa bora ni ile inayotokana na ridhaa ya watu wawili wanaopendana na kukubaliana kufunga ndoa kwa hiari yao, badala ya kulazimishwa au kuchaguliwa wenza.

Lulu ameeleza kuwa “Uamuzi wa kufunga ndoa ni jambo linalopaswa kutoka moyoni mwa wahusika wenyewe, akiamini kuwa kila mmoja anapaswa kuwa tayari kuingia katika maisha ya ndoa bila shinikizo kutoka kwa watu wengine.

Amesema “Ndoa zinazofungwa kwa kulazimishana zinaweza kukumbwa na changamoto kubwa ikilinganishwa na zile ambazo wahusika wameamua wenyewe kuishi pamoja kwa ridhaa na makubaliano yao.

Mbali na suala la ndoa, msanii huyo pia amesisitiza”Kuna umuhimu wa kumpa mtu uhuru wa kuamua wakati sahihi wa kupata mtoto, akieleza kuwa maamuzi hayo hayapaswi kuamuliwa na shinikizo la jamii au watu wanaomzunguka.

Lulu ameeleza kuwa ingawa alitamani kupata watoto mapema, alitaka kwanza kuhakikisha kuwa watoto wake wangekulia katika mazingira yenye msingi imara wa maisha, tofauti na changamoto alizopitia yeye huko nyuma.

Aidha, amesema moja ya mambo aliyoyazingatia ni kuhakikisha watoto wake wanapata malezi kutoka kwa wazazi wote wawili, baba na mama, ili wakue katika mazingira yenye uwepo na ushiriki wa wazazi wao.

Mtazamo huo wa Lulu unakuja katika kipindi ambacho maisha yake ya kimapenzi na familia yameendelea kuwa sehemu ya mambo yanayowavutia mashabiki wake.

Msanii huyo amekuwa katika uhusiano na Majizzo kabla ya wawili hao kufunga ndoa yao kwa faragha kanisani, takribani miaka mitano baadaye, bila kufanya sherehe kubwa ya harusi.

Kwa sasa, Lulu na Majizzo wamejaliwa kupata watoto wawili. Mara kadhaa, wawili hao wamekuwa wakionesha upendo wao kwa watoto wao, huku maisha yao ya familia yakiendelea kuonekana kupitia nyakati mbalimbali wanazoshiriki.

Kauli ya Lulu inaibua mjadala kuhusu umuhimu wa ridhaa katika ndoa, uhuru wa kufanya maamuzi ya kifamilia na wajibu wa wazazi katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira yenye upendo na malezi bora.

Related Articles

Back to top button