JKT Tanzania yaipa Azam mtihani

DAR ES SALAAM: JKT Tanzania imesema inalenga kuifunga Azam FC katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Oktoba 31, 2026, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, ili kupanda zaidi katika msimamo wa ligi hiyo.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa JKT Tanzania, Masau Bwire, amesema wanatambua ugumu wa kukutana na Azam FC, lakini wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanapata pointi tatu zitakazowawezesha kuimarisha nafasi yao katika msimamo wa ligi.
JKT Tanzania inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza mechi 10, sawa na Azam FC ambayo ina pointi hizo baada ya kucheza mechi nane. Yanga inashika nafasi ya pili kwa pointi 22, huku Simba ikiongoza kwa pointi 24, zote zikiwa zimecheza mechi nane.
Bwire amesema Azam ni miongoni mwa timu kubwa zilizowekeza katika soka na zenye malengo makubwa, lakini JKT Tanzania ina kikosi chenye uwezo wa kushindana na timu yoyote na kupata matokeo chanya.
“Benchi la ufundi chini ya kocha Ahmed Ally linaendelea kuandaa mbinu na mikakati ya kukabiliana na Azam, maandalizi hayo yanalenga kuthibitisha ubora wa kikosi chetu na kuongeza ushindani katika ligi,”amesema.
JKT Tanzania inaingia katika mchezo huo baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Bwire amesema ushindi dhidi ya Azam utakuwa hatua muhimu kabla ya kukutana na Simba Sports Club na baadaye Singida Black Stars.
Amesisitiza kuwa michezo hiyo mitatu ni sehemu ya dhamira ya JKT Tanzania kujijengea heshima na kusogea kuelekea kileleni mwa msimamo wa ligi, akieleza kuwa timu hiyo inaamini inaweza kupata matokeo mazuri hata dhidi ya wapinzani wenye ushindani mkubwa.




