Filamu

Tom Cruise kutunukiwa tuzo ya heshima katika filamu

LONDON: MWIGIZAJI na mtayarishaji maarufu wa Hollywood, Tom Cruise, anatarajiwa kutunukiwa tuzo ya 52 ya AFI Life Achievement Award kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia ya filamu.

Taasisi ya American Film Institute (AFI) ilitangaza kuwa tuzo hiyo itakabidhiwa Aprili 24, 2027, katika hafla maalumu itakayofanyika ukumbi wa Dolby Theatre jijini Los Angeles, Marekani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya AFI, Kathleen Kennedy, alimwelezea Cruise kama nyota wa kimataifa mwenye kujituma katika kazi zake za uigizaji na utayarishaji wa filamu.

Kennedy alisema pia kuwa imani yake kubwa katika uwezo wa filamu kuwaunganisha watu imemfanya kuwa balozi muhimu wa sinema za Marekani duniani.

Cruise ni miongoni mwa waigizaji wanaotambulika zaidi duniani, akiwa na kazi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 50. Ameigiza katika filamu zilizopata umaarufu mkubwa, zikiwemo ‘Top Gun’, ‘Rain Man’, ‘A Few Good Men’, ‘Jerry Maguire’, ‘Minority Report’ na ‘The Last Samurai’, pamoja na mfululizo wa filamu za ‘Mission: Impossible’.

Katika safari yake ya kisanii, Cruise amepata uteuzi kadhaa wa tuzo za Oscar. Aliteuliwa kama mwigizaji bora wa kiume kupitia filamu ‘Born on the Fourth of July’ na ‘Jerry Maguire’, huku akipata uteuzi wa mwigizaji bora msaidizi kupitia ‘Magnolia’. Pia aliteuliwa kama mtayarishaji katika kipengele cha filamu bora kupitia Top Gun: Maverick katika tuzo za Oscar za mwaka 2022.

Mwaka 2025, Cruise alitunukiwa Oscar ya heshima katika hafla ya Governors Awards, kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya tasnia ya filamu. Waigizaji wengine waliowahi kupokea tuzo ya AFI Life Achievement Award ni pamoja na Eddie Murphy, Nicole Kidman, Julie Andrews, Denzel Washington na George Clooney.

Kwa sasa, Cruise pia anazungumziwa kutokana na filamu yake mpya, Digger, iliyoongozwa na Alejandro González Iñárritu. Katika filamu hiyo, anacheza nafasi ya Digger Rockwell, tajiri wa mafuta mwenye tabia za kipekee ambaye ajali ya uchimbaji mafuta baharini nchini Greenland inasababisha janga la kimazingira duniani. Muonekano wake usio wa kawaida katika filamu hiyo umeongeza hamu ya mashabiki kutaka kuona kazi hiyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button