Carrick hahofii kutimuliwa United

COMO: LICHA ya Kocha wa Manchester United, Michael Carrick kukiri matokeo ya kufungwa na Como mabao 4-1 hayakubaliki lakini amesisitiza hana hofu ya kupoteza nafasi yake katika klabu hiyo.
United ikiwa ugenini jana Jumatano Uwanja wa Giuseppe Sinigagli, ilizidiwa ujanja na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza na kuendeleza vipigo vya aibu mfululizo.
Kichapo hicho kimeendeleza rekodi ya United kutopata ushindi kwenye mechi saba mfululizo za michuano yote mpaka sasa.
Kwa sasa nafasi ya Carrick ipo kwenye uangalizi mkali kufuatia mwenendo mbaya wa timu, ambao unajumuisha kuanza msimu wa ligi kwa namna mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 40.
Hata hivyo, mwisho wa mechi hiyo, Carrick aliwafuata mashabiki waliokuja kuwaunga mkono na kuwaomba radhi kwa kilichotokea.
“Sijawahi hata kufikiria kuhusu nafasi yangu. Na siku zote huwa nawaendea mashabiki, bila kujali hali ilivyo.
“Hakukuwa na sababu maalum tofauti iliyonifanya niwaendee. Ni ishara ya kuonesha shukrani na kutambua magumu waliyopitia, pamoja na mambo waliyofanya katika kipindi cha wiki chache zilizopita. Hasa hasa usiku wa leo (jana).”
Como chini ya Cesc Fabregas ilijipatia uongozi wa mabao 4-0 kabla ya mchezaji wa akiba Joshua Zirkzee kufunga bao la kufutia machozi katika muda wa nyongeza.
“Kucheza kwa namna ile, si jambo linalokubalika. Haikuwa kiwango kizuri hata kidogo. Tulitaka kuendeleza kile tulichoonyesha na kiwango tulichokuwa nacho dhidi ya Leeds.
“Ile hali ya kujituma, ule moyo wa kupambana, ile nguvu, na ile nia ya dhati ya kutoa kila kitu, leo tuliona kinyume kabisa cha hayo. Lazima niseme, ilikuwa vigumu kutazama,” alisema Carrick.




