
DIDIER Deschamps ametangaza kuwa ataacha kuifundisha timu ya taifa ya Ufaransa baada ya Kombe la Dunia la 2026, akihitimisha enzi kubwa katika historia ya soka ya taifa hilo. Deschamps, aliyeteuliwa mwaka 2012 baada ya Laurent Blanc kujiuzulu, aliongoza Ufaransa kushinda Kombe la Dunia la 2018, kufika fainali ya 2022, na pia fainali ya Euro 2016.
Amesema kuwa, “Nimekuwa hapa tangu 2012, nimepangiwa hadi 2026. Inapaswa kuishia hapo. Kuna maisha baada ya ukocha.”
Kwa miaka 14, Deschamps amekuwa na mafanikio makubwa, lakini pia amekosolewa na mashabiki kwa mtindo wake wa kucheza wa kujihami licha ya kuwa na washambuliaji wengi wenye talanta kubwa. Hata hivyo, mafanikio yake ya mataji na asilimia ya ushindi ya asilimia 64.2 yanamuweka miongoni mwa makocha bora wa kimataifa.
Zinedine Zidane, aliyekuwa mchezaji mwenzake katika ushindi wa Kombe la Dunia 1998, anatajwa kuwa chaguo kuu la kumrithi. Zidane, ambaye aliongoza Real Madrid kushinda Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo, amekuwa bila kazi tangu 2021 alipoondoka Madrid.
Katika historia yake ya ukocha, Deschamps pia aliwahi kuiongoza Monaco kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2004 na kuisaidia Juventus kupanda tena Serie A baada ya kashfa ya Calciopoli. Alipokuwa Marseille, aliwapatia taji la Ligue 1 msimu wa 2009-10, mafanikio ambayo hayajarejewa tena na klabu hiyo tangu wakati huo.
Deschamps ataondoka huku akitambulika kama mmoja wa makocha wenye mafanikio makubwa, akiwemo kundi la kipekee la watu waliofanikiwa kushinda Kombe la Dunia kama mchezaji na kocha.