Yanga yaingia mawindoni kimya kimya

DAR ES SALAAM: YANGA imeingia mawindoni kimya kimya, ikiendelea na maandalizi ya kuwania ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CFFA ya Madagascar utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Wananchi wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kiu ya kurejesha furaha kwa mashabiki wao baada ya kupoteza mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwishoni mwa wiki iliyopita.
Matokeo hayo yameongeza umuhimu wa mchezo wa Jumamosi kwa Yanga, ambayo inahitaji kuonesha mwitikio ndani ya uwanja na kuanza ukurasa mpya kwa matokeo yatakayowapa nguvu ya kuendelea na safari yao ya kimataifa.
Hata hivyo, badala ya kufanya maandalizi yao kwa makelele mengi, kikosi hicho kinaendelea kujifua kwa utulivu, kikilenga kuweka mambo sawa kabla ya kukutana na mpinzani wake katika mashindano hayo ya klabu barani Afrika.
Kwa Yanga, mchezo huo ni nafasi ya kugeuza maumivu ya kipigo cha debi kuwa motisha ya kupambana, huku ikifahamu kuwa mashabiki wake wanatarajia kuona timu ikirejea kwenye kiwango cha ushindani na kupata matokeo chanya.
Timu hiyo inakabiliwa na changamoto ya kurejesha uimara wake, hasa katika eneo la kiungo, baada ya kocha Manqoba Mngqithi kueleza kuwa kupoteza udhibiti wa eneo hilo kulichangia matokeo mabaya dhidi ya Simba.
Tayari wapinzani wa Yanga wameshawasili Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo huo muhimu utakaoweka taswira juu ya hatma yao ya kusonga mbele hatua ya makundi.




