Mastaa

Shakib Cham alalamikia malipo madogo ya Facebook

KAMPALA: MFANYABIASHARA kutoka Uganda, Shakib Cham, amezua mjadala baada ya kulalamikia kiasi kidogo cha fedha alicholipwa na Facebook licha ya maudhui yake kupata mamilioni ya watazamaji.

Katika kipindi cha siku saba hadi Oktoba 5, ukurasa wake ulifikisha watazamaji milioni 11, huku ukipata zaidi ya mwingiliano 967,000 na wafuasi wapya 6,415. Hata hivyo, Shakib alisema alipokea takribani Sh334,000 pekee.

Akilalamikia mfumo huo, Shakib alimtaja mwanzilishi wa Meta, Mark Zuckerberg, akitaka maelezo kwa nini mapato yake yalikuwa madogo licha ya idadi kubwa ya watazamaji.

Hii si mara ya kwanza kwa Shakib kuhoji malipo ya Facebook. Mwezi Agosti alionesha takwimu za chapisho lililofikisha watazamaji milioni 41 na mwingiliano milioni 2.1, lakini mapato yake yalikuwa takribani Sh2.8 milioni pekee.

Wataalamu wa masoko mtandaoni wameeleza kuwa kiasi cha malipo hutegemea mambo mbalimbali, ikiwemo eneo walipo watazamaji, kwa kuwa thamani ya matangazo hutofautiana kati ya soko moja na jingine.

Licha ya kulalamikia Facebook, Shakib amesema mapato kutoka jukwaa hilo ni sehemu ndogo tu ya kipato chake, huku akipata fedha zaidi kupitia biashara zake, ikiwemo King Cham Collection, uuzaji wa magari na biashara ya madini.

Related Articles

Back to top button