Harmonize, Cristina kumechangamka kwelikweli

ZANZIBAR: MSANII Harmonize ameendelea kugonga vichwa vya habari kwa yanayoendelea baina yake na video vixen wa video ya wimbo wake wa Kudos, Cristina Celi.
Cristina anayetajwa ‘kutoka’ na Harmo ameweka video mtandaoni ya msanii huyo akiwa analia huku akisisitiza asifanyiwe hivyo.
Mrembo huyo anaonekana akimbembeleza bosi huyo wa Lebo ya Konde Gang ambaye naye anafafanua kuwa analia kwa ajili ya Cristina na kwamba si vyema anachomfanyia.
Hata hivyo, video hiyo ikasindikizwa na ujumbe: “Sikupanga kuzungumza chochote kwa yaliyotokea lakini unanivunjia heshima, sitakaa kimya na kuruhusu hilo. Video itafuata, yaani kama vile hukuniomba nije kwako tumalize vitu sababu hukutaka tumalize hivi.”
Kama hiyo haitoshi, Cristina akaweka ujumbe mwingine mtandaoni akieleza yeye sio wa kuvunjiwa heshima na kukaa kimya ila atamwonesha namna gani wanawake wa Marekani hawakai kimya wakivunjiwa heshima.
Akaenda mbali zaidi na kueleza sasa ameelewa kwa nini watu humuonea huruma mpenzi wa zamani wa Harmo, Kajala Masanja na kisha kusisitiza bado mengi yatafuata kwani yeye anaweza kuucheza huu mchezo.
Awali, kabla ya kuibuka hayo, ilivuja video inayowaonesha wawili hao wakihitirafiana, ikielezwa Cristina ametoa takriban Sh milioni 10 kwenye ‘ATM’ kupitia kadi ya benki ya Harmonize, kinyume na matakwa ya msanii huyo, tukio ambalo lilihusisha polisi pia.
Lakini hivi karibuni, Harmo au Tembo alipohojiwa kuhusiana na vurumai hizo alisema yeye ameegemea zaidi kutengeneza muziki na watu wasiwe na wasiwasi kwani video hiyo inaweza kuwa ni sehemu ya ‘Kudos screen version’.




