Africa

Ghana yamfuta kazi kocha mkuu

ACCRA: SHIRIKISHO la Soka Ghana (GFA) limevunja mkataba na kocha wa timu ya taifa, Carlos Queiroz baada ya kuanza vibaya kampeni ya kufuzu Kombe la Mataifa Afrika 2027 (AFCON).

Imeelezwa hilo limejiri leo Alhamisi baada ya kikao cha shirikisho hilo na kocha huyo raia wa Ureno aliyekiongoza kikosi hicho katika mechi saba pekee.

Katika mechi mbili za mwisho, Ghana imefungwa na Ivory Coast mabao 2-0 kisha kuchapwa na Gambia mabao 4-2.

Matokeo hayo yameiacha timu hiyo mkiani mwa Kundi C na katika hatari ya Ghana kuikosa AFCON kwa mara ya pili mfululizo.

Queiroz amesema alifika Ghana akiwa na lengo la kujenga msingi imara kwa ajili ya mustakabali wa timu hiyo, lakini matokeo ya hivi karibuni na mazingira yaliyokuwepo yamechangia uamuzi wa kumaliza ushirikiano huo.

“Imekuwa heshima kubwa kuitumikia Ghana na timu ya Black Stars. Ninatoa shukrani za dhati kwa shirikisho la Ghana na hasa rais wake kwa imani yao na kwa kunipa fursa ya kuiongoza nchi yenye fahari kubwa katika soka.

“Nilikuja Ghana nikiwa na azma ya kusaidia kujenga mustakabali imara zaidi kwa Black Stars na kusaidia kukuza vipaji vya nchi. Licha ya kujitolea na juhudi zetu, mazingira muhimu hayakuwepo kikamilifu, na kiwango chetu cha hivi karibuni kilichangia katika uamuzi wa kuhitimisha safari hii,” alisema kocha huyo wa zamani wa Colombia.

Mbali na mechi hizo mbili za kufuzu AFCON, Queiroz alianza kuiongoza Ghana Juni, mwaka huu katika sare ya 1-1 dhidi ya Wales kwenye mechi ya kirafiki.

Kisha kwenye Kombe la Dunia 2026, alipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Panama, kabla ya suluhu dhidi ya England na kisha kupoteza mbele ya Croatia na Colombia kwenye Kundi L.

Related Articles

Back to top button