Kwingineko

Ligi Kuu Kenya yapigwa ‘stop’

MURANG’A: LIGI Kuu ya Kenya iko hatarini kutoanza kuunguruma kesho Jumamosi baada ya kesi mpya iliyoibuliwa Mahakama ya Murang’a dhidi ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

Vyombo vya habari Kenya vimeripoti kuwa Evans Nduta ndiye aliyepeleka kesi hiyo mpya mahakamani na viongozi wa FKF walitarajiwa kufika mahakamani leo Ijumaa kujua hatma ya ligi hiyo.

Awali, kulikuwa na sintofahamu ya ligi hiyo baada ya mkanganyo wa timu zinazopanda daraja baina ya Kariobangi Sharks na Mombasa United, lakini mahakama ikaruhusu ligi kuendelea wakati timu hizo zikitafuta mwafaka kwenye mamlaka husika.

Baadaye, FKF na klabu shiriki zilikubaliana Septemba 19, mwaka huu ligi hiyo ianze sanjari na makubaliano kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni na mahitaji ya kimatibabu siku ya mechi.

Inaelezwa kuwa mtafaruku ulianzia kwenye mabishano ya mabadiliko ya kanuni ya mwaka 2019 na 2025 zinazoeleza mfumo utakaotumika kupata timu zitakazopanda daraja kushiriki Ligi Kuu.

Mtandao wa SpotiLeo umezungumza moja kwa moja na mdau mkubwa wa soka Kenya, Augustine Ramaita ambaye alieleza masikitiko yake juu ya sarakasi hizo na mwelekeo wa athari za soka la Kenya msimu huu.

“Ni pigo kwa kweli, timu zimeshajitayarisha kwa ajili ya ligi na watu wako tayari lakini sasa hatuelewi kinachoendelea.

“Pia kuna ishu ya maandalizi ya Afcon (Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika), sasa hii inaathiri pia hilo, waru wengi inawatoa mchezoni hasa ukizingatia kila mtu anataka soka lichezwe,” alisema Ramaita.

Aidha, mitandao na wadau mbalimbali Kenya wanahoji ni maslahi ya nani yanayowakilishwa na maombi hayo ya Evans Nduta, wakijiuliza uhalali wa ligi nzima kuwa na vurugu wakati mahakama ilishatoa mwongozo wa ligi kuendelea wakati masuala yenye utata yakishughulikiwa.

 

Related Articles

Back to top button