Muziki

Clark ataka uchunguzi huru kifo cha Takeoff

TEXAS: Patrick Xavier Clark anayeshtakiwa kwa kifo cha rapa Takeoff, ameiomba mahakama iruhusu ushahidi wa kesi hiyo uchunguzwe na mtaalamu huru.

Kulingana na makabrasha ya mahakamani yaliyonaswa na Mtandao wa TMZ, yanaeleza uchunguzi huo uanzie katika Idara ya Polisi ya Houston ikiwemo risasi zinazodaiwa kuhusishwa na tukio la Takeoff la mwaka 2022.

Clark analitaka hilo lifanyike kabla ya kuanza rasmi kusikilizwa kwa kesi hiyo Novemba, mwaka huu.

Mtuhumiwa huyo anakanusha kuhusika na kifo cha rapa huyo aliyekuwa Kundi la Migos.

Na zaidi anataka uchunguzi huo huru ufanyike ili hata upande wake uwe na uwezekano wa kuhoji au kupinga ushahidi unaotumika dhidi yake.

Clark, 33 alikamatwa na polisi Desemba, 2022 baada ya kifo cha Takeoff kilichojiri Novemba Mosi, mwaka huo.

Takeoff aliyefariki akiwa na miaka 28 alipigwa risasi na kufariki papo hapo akiwa na memba mwenzake wa Migos, Quavo dakika chache baada ya kuibuka mabishano sehemu waliyokuwa wamekaa wao.

 

Related Articles

Back to top button