Ngorongoro heroes kuivaa Rwanda Cecafa

DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inaanza safari ya kuwania tiketi ya Fainali za AFCON 2027 itakayofanyika Ghana, ikifungua kampeni yake kwa kukutana na Rwanda katika mchezo wa Kanda ya CECAFA utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, saa 2:00 usiku.
Kocha wa Ngorongoro Heroes, Mario Campesino, amesema licha ya kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu Rwanda, timu yake imejikita katika kuboresha mchezo wake na kuhakikisha inatawala pambano hilo ili kuanza kampeni kwa ushindi.
“Maandalizi yetu kuelekea mchezo dhidi ya Rwanda yamejikita kwenye timu yetu. Tunajiandaa kujaribu kuutawala mchezo na kushinda. Hatujui mpinzani yukoje, hatuna taarifa zake na wao pia hawana taarifa kuhusu sisi,” amesema Rivera.

Amesema hali hiyo imewafanya kuzingatia zaidi falsafa yao ya uchezaji na kujiandaa kukabiliana na aina yoyote ya mchezo ambao Rwanda inaweza kuja nao, huku lengo likiwa ni kutawala mchezo na kutafuta ushindi.
Kocha huyo pia amewatoa hofu mashabiki kuhusu utayari wa kikosi chake, akisema wachezaji wote wako tayari na ushindani wa nafasi kwenye kikosi cha kwanza umeongeza morali katika maandalizi yao.
Mchezo huo ni mwanzo wa safari ya Ngorongoro Heroes katika harakati za kutafuta nafasi kwenye AFCON U-20 ya 2027, huku mataifa tisa kutoka Kanda ya Afrika Mashariki na Kati yakishindania nafasi mbili za kufuzu kwenye michuano hiyo mikubwa ya vijana.
Kwa Ngorongoro Heroes, ushindi wa leo utakuwa mwanzo muhimu wa safari hiyo, hasa katika mashindano ambayo kila pointi inaweza kuwa na thamani kubwa katika mbio za kutafuta tiketi mbili za kwenda Ghana.
Michezo mingine ni Uganda dhidi ya Djibouti huku Sudan Kusini ikitarajia kucheza dhidi ya Burundi.




