Kila taji la Miss Tanzania 2026 ‘litasomesha watoto 100’

DAR ES SALAAM: MWANDAAJI wa Shindano la Miss Tanzania 2026, Leah Lwendamseke ‘Lamata’, amesema kila taji litakalotolewa katika mashindano hayo litasaidia kusomesha takribani watoto 100, ikiwa ni sehemu ya kutumia jukwaa hilo kuleta matokeo chanya katika jamii.
Lamata amesema hayo baada ya kuzindua rasmi msimu mpya wa kusaka washiriki wa Miss Tanzania 2026 kupitia kanda saba nchini, katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Amesema dhamira ya mashindano hayo ni kwenda mbali zaidi ya urembo kwa kutumia jukwaa la Miss Tanzania kutoa fursa, kuwawezesha vijana na kuchangia maendeleo ya jamii.
Aidha, amewaomba wazazi nchini kutoa ushirikiano na kuwaunga mkono mabinti wao wenye nia na sifa za kushiriki katika mashindano hayo, akisisitiza kuwa mfumo mpya wa Miss Tanzania unalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kukabiliana na maisha na kutumia fursa mbalimbali zinazowazunguka.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Kamati ya Miss Tanzania 2026, Grace Mgaya, amesema mashindano ya mwaka huu yatafanyika katika kanda saba nchini kwa lengo la kufikia vijana wengi zaidi na kuibua vipaji kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Msemaji wa Kamata Village, Grace, amesema Miss Tanzania 2026 imekuja na mfumo mpya unaolenga kuwapa washiriki fursa zaidi ya mashindano ya urembo.
Amesema washiriki na washindi watapatiwa mafunzo mbalimbali, yakiwamo ya elimu na ujuzi wa shughuli tofauti za kimaisha, kwa lengo la kuwajengea uwezo, kujiamini na kuwaandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali.
“Tunataka Miss Tanzania isiwe jukwaa la urembo pekee, bali iwe sehemu ya kuwawezesha vijana, kuwajengea uwezo na kuwapa nafasi ya kutoa mchango chanya katika maendeleo ya jamii,” amesema Grace.
Mfumo huo mpya, kwa mujibu wa waandaaji, unatarajiwa kuipa Miss Tanzania sura mpya inayounganisha urembo, elimu, vipaji na uwajibikaji wa kijamii.




