Shime: Bado tuna nafasi Kombe la Dunia

BIELSKO BIALA: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania, Tanzanite Queens, Bakari Shime amesema licha ya timu hiyo kupoteza michezo miwili ya kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la Wanawake U-20 nchini Poland, bado wana nafasi ya kusonga mbele na wataingia uwanjani leo, Septemba 11, 2026, wakilenga ushindi dhidi ya Canada.
Tanzanite Queens imepoteza michezo miwili dhidi ya Brazil kwa mabao 4-1 na England kwa mabao 5-1, huku Canada ikiwa na pointi moja baada ya kutoka sare ya 1-1 na England na kupoteza 0-3 dhidi ya Brazil.
Akizungumzia mchezo huo, Shime amesema kikosi chake kimechukua matokeo ya michezo iliyopita kama sehemu ya kujifunza na sasa kimejikita katika mchezo huo wa mwisho wa kundi, ambao ushindi unaweza kuwapa nafasi ya kuendelea na mashindano.
“Tumeshapata matokeo mawili, tumeyachukua kama fundisho. Mchezo wa kwanza tumepoteza, mchezo wa pili tumepoteza, lakini tuna mechi nyingine ya tatu na ya mwisho (leo). Bado tuna nafasi ya kusonga mbele kwenye shindano na tumejiandaa kucheza vizuri, kushinda na kupata fursa ya kusonga mbele,” amesema Shime.
Shime amesema wamefanya uchambuzi wa namna Canada ilivyocheza katika michezo yake miwili iliyopita ili kubaini mbinu ambazo wanaweza kuzitumia kuwadhibiti wapinzani hao, huku pia wakitafuta namna ya kuwashambulia watakapokuwa na mpira.
Mchezo huo utakaochezwa katika Uwanja wa Miejski, Bielsko-Biała, ni wa mwisho kwa timu zote mbili katika Kundi B, huku Canada ikiwa na pointi moja na Tanzania ikiwa haina pointi. Canada ilitangaza awali kuwa michezo yake yote ya hatua ya makundi ingechezwa katika uwanja huo.
Kwa mfumo wa mashindano hayo, timu mbili za juu kutoka kila kundi zitasonga mbele moja kwa moja, huku nafasi nne zaidi zikichukuliwa na timu bora zitakazomaliza katika nafasi ya tatu. Hivyo, Tanzania inahitaji ushindi dhidi ya Canada na kisha kusubiri matokeo ya makundi mengine ili kujua kama itapata nafasi ya kuingia hatua ya 16 bora.
Shime amewataka wachezaji wake kutumia mchezo huo kama fursa ya kuonesha uwezo wao na kupigania matokeo yatakayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kuendelea na mashindano.




