Kagera Sugar yauwazia mchezo wa Mashujaa

KIGOMA: KAGERA Sugar wametua Kigoma tayari kwa mchezo dhidi ya Mashujaa utakaochezwa kesho huku uongozi wa timu hiyo ukisema wamefanya maandalizi mazuri tayari kwa kuwakabili wapinzani.
Ofisa Habari wa Kagera Sugar Stephen Julius amesema kuwa hali ya kikosi ni nzuri, isipokuwa wachezaji kadhaa wanaendelea na matibabu kutokana na majeraha.
“Tunashukuru Mungu tumefanya maandalizi makubwa sana kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mashujaa. Tunaamini hautakuwa mchezo rahisi kutokana na Mashujaa kupoteza mchezo wao wa mwisho, lakini pia sisi mchezo wetu wa mwisho pale Geita haukuwa mzuri,” amesema.
Kocha huyo amesema licha ya kuwa na majeruhi kadhaa, hali zao si ya kutisha na baadhi yao wanaweza kuwa kwenye mpango wa mchezo huo.
“Tuna majeruhi kama wanne, lakini kwa bahati nzuri majeraha yao yapo kwenye mpango wa mechi husika. Kwa hiyo niseme tu kikosi kiko vizuri,” amesema.
Kagera Sugar ni miongoni mwa timu sita ambazo hazijapata ushindi katika mechi za mwanzo zaidi ya sare moja na kupoteza michezo miwili hivyo huenda ukawa katika presha kubwa ya kupambania ushindi.



