Mwanamitindo Bora wa Afrika 2026 kusakwa

NAIROBI: Wizara ya Utalii na Wanyamapori nchini Kenya imeidhinisha rasmi mashindano ya Mwanamitindo Bora wa Afrika 2026 ‘Africa’s Next Super Model 2026’, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kukuza sekta ya mitindo, ubunifu na vipaji barani Afrika.
Uungwaji mkono huo pia unaimarisha nafasi ya Afrika kama kituo muhimu cha utalii, vipaji vya mitindo inayolenga soko la kimataifa.
Kampeni ya kutafuta vipaji vipya inaanza rasmi Agosti 29, 2026, jijini Nairobi, ikiwa na lengo la kumpata mwanamitindo wa Afrika mwenye uwezo wa kufanya vizuri katika majukwaa makubwa ya kimataifa.
Baada ya kuanza Nairobi, zoezi la usaili na uchukuaji vipimo (casting) litaendelea hadi mwisho wa Septemba katika maeneo mbalimbali nchini Kenya.
Waandaaji wamepanga kufikisha zoezi hilo nje ya miji mikubwa, likiwemo kufanyika katika maeneo yenye jamii za Turkana na Maasai, ili kuhakikisha vipaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi vinapata nafasi ya kuonekana.
Zoezi hilo linatarajiwa kuwahusisha wanamitindo kutoka Kenya pamoja na mataifa mengine ya Afrika, yakiwemo Angola, Côte d’Ivoire, Togo, Benin, Ghana, Rwanda, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini na Ethiopia.
Akizungumza kuhusu uungwaji mkono wa Wizara na kampeni hiyo, Katibu Mkuu wa Utalii na Wanyamapori, Julius Bitok, amewahimiza wasichana wa Kenya wenye umri wa kati ya miaka 18 na 26 kutumia fursa hiyo kujitokeza na kujaribu bahati yao.
Bitok amesema mpango huo unaweza kuwa jukwaa muhimu kwa vijana wenye vipaji wanaotamani kupata nafasi katika tasnia ya mitindo ya kimataifa.
Kinara wa mpango huo ni Joan Okorodudu, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Isis Models International, ambaye pia ndiye mwanzilishi wa Africa’s Next Super Model.
Kupitia mpango huo, Okorodudu analenga kuibua na kukuza vipaji vya wanamitindo kutoka Afrika na kuwapa fursa ya kufikia soko la kimataifa.
Kwa kuhusisha maeneo mbalimbali ya bara hilo, Africa’s Next Super Model 2026 inalenga kuwa zaidi ya shindano la uanamitindo, bali jukwaa la kuunganisha vipaji vya Afrika na sekta ya mitindo ya kimataifa.
Kwa Kenya, hatua hiyo inatoa fursa ya kuunganisha utalii, utamaduni, ubunifu na mitindo huku ikiiweka nchi katika nafasi ya kuwa mwenyeji wa matukio makubwa yanayolenga kukuza vipaji vya Afrika.




