Muziki

Luizer Mbutu: Twanga Pepeta imeajiri zaidi ya familia 40

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa dansi nchini, Luizer Nyoni Mbutu, amempongeza na kumshukuru Asha Baraka kwa mchango wake katika kuendeleza muziki wa dansi, akisema kupitia Bendi ya Twanga Pepeta ameweza kutoa ajira kwa zaidi ya familia 40.

Luizer amesema Asha Baraka ni mwanamke mwenye juhudi na asiyekata tamaa, akieleza kuwa amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha bendi hiyo inaendelea kutoa burudani na wakati huo huo kuwa chanzo cha ajira kwa wasanii na wafanyakazi mbalimbali.

Akizungumzia mchango wa Asha Baraka, Luizer amesema licha ya kuwa mwanamke, ameonesha uwezo mkubwa katika kusimamia na kuendeleza shughuli za muziki wa dansi.

“Ni mwanamke na nusu, ni mpambanaji asiyekata tamaa. Leo hii ni Mbunge wa Viti Maalumu, amepambana kwa miaka mingi hadi kupata nafasi hiyo, lakini pia ameipigania Bendi ya Twanga Pepeta kwa muda mrefu,” amesema Luizer.

Amesema mafanikio ya Twanga Pepeta hayapaswi kuangaliwa katika upande wa burudani pekee, bali pia katika nafasi ambayo bendi hiyo imekuwa nayo ya kutoa ajira na kuwawezesha wasanii pamoja na familia zao kupata kipato.

Kwa mujibu wa Luizer, kazi kubwa inayofanywa na Asha Baraka ni mfano wa namna sanaa inavyoweza kuwa sehemu muhimu ya uchumi na kusaidia maisha ya watu wengi.

Amesema juhudi za kuendeleza muziki wa dansi zinapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wasanii wanapata nafasi zaidi za kufanya kazi na kujenga maisha yao kupitia vipaji walivyonavyo.

Luizer ametoa pongezi hizo huku akisisitiza umuhimu wa kutambua mchango wa watu wanaowekeza katika sanaa na kuhakikisha muziki wa dansi unaendelea kuwa sehemu ya ajira na burudani nchini.

Related Articles

Back to top button