Nandy na Billnass wanafaika na kilimo

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’, amefunguka kuhusu safari yake ya uwekezaji na biashara, akieleza jinsi yeye na mume wake, William Lyimo ‘Billnass’, walivyoamua kuwekeza katika sekta ya kilimo na kuanza kuona matunda ya juhudi zao.
Nandy amesema kwa sasa wao ni miongoni mwa wasanii wanaonufaika na shughuli za kilimo baada ya kujikita katika sekta hiyo kwa takribani miaka mitatu.
Akizungumza kuhusu safari hiyo, Nandy amesema haikuwa rahisi kwani walikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo hasara na kushindwa kufanikiwa katika baadhi ya miradi waliyoianzisha.
Ameeleza kuwa licha ya vikwazo hivyo, hawakuruhusu changamoto hizo kuwakatisha tamaa, badala yake waliamua kujifunza kutokana na makosa yao na kuendelea kutafuta mbinu bora zaidi za kufanikisha uwekezaji wao.
“Tumepitia mengi kwenye safari hii. Kuna wakati tulipata hasara na kufeli kwenye baadhi ya miradi, lakini hatukukata tamaa. Tuliendelea kujifunza na kujaribu tena,” amesema Nandy.
Msanii huyo amesema hatua kwa hatua juhudi zao zimeanza kuzaa matunda, huku wakipata kipato kupitia shughuli za kilimo walizowekeza.
Nandy amebainisha kuwa mafanikio katika biashara hayaji kwa haraka kama wengi wanavyofikiria, bali yanahitaji uvumilivu, uthubutu na utayari wa kujifunza hata pale unapopata hasara.
Akiwahamasisha vijana na Watanzania kwa ujumla kuingia kwenye uwekezaji, Nandy alisema ni muhimu kutokuwa na hofu ya kujaribu fursa mpya zinazoweza kubadilisha maisha.
“Usiogope kujaribu,” amesema.
Kwa mujibu wa Nandy, siri ya mafanikio ni kuendelea kusimama kila unapokutana na changamoto na kutokubali kushindwa kukuzuie kufikia malengo yako.
Kauli yake imepokelewa kama somo muhimu kwa vijana wengi wanaotamani kuingia katika biashara na uwekezaji, huku ikionyesha kuwa pamoja na umaarufu wao kwenye muziki, Nandy na Billnass wameamua pia kujenga mustakabali wao kupitia sekta ya kilimo, ambayo imeendelea kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi nchini.
Safari yao inaonesha kuwa mafanikio ya kweli yanahitaji muda, uvumilivu na dhamira ya kuendelea mbele licha ya changamoto zinazojitokeza njiani.




