Mastaa

Jaji wa American Got Talent, Sidemen waachana

MMOJA wa majaji wa American Got Talent na nyota wa mtandaoni (YouTuber), Olajide Olayinka maarufu kama KSI ametangaza kuondoka katika kundi la Sidemen baada ya miaka 13 ya ushirikiano wao.

Jaji huyo ambaye pia ni mwanamuziki, mfanyabiashara, na mwanamasumbwi wa Uingereza, walianzisha kundi hilo tangu mwaka 2013, amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Sidemen kupitia video za soka, vichekesho na changamoto mbalimbali zilizowavutia mamilioni ya watazamaji duniani.

Tangazo la kuondoka kwake limekuja baada ya wiki kadhaa za uvumi, huku mashabiki wengi wakidhani kuwa ilikuwa ni mbinu ya kutafuta umaarufu. Hata hivyo, msemaji wake alithibitisha kuwa uamuzi huo ni wa kweli.
KSI amesema majukumu yake mengi katika muziki, biashara, ndondi na miradi mingine yamefanya iwe vigumu kuendelea kutoa muda wa kutosha kwa Kundi hilo.

“Nimefikiria kwa muda mrefu kuhusu jambo hili. Hakuna mgogoro wowote, ni uamuzi wa binafsi unaotokana na majukumu mengi niliyonayo kwa sasa,” alisema.

Kwa upande wao, wanachama wa Sidemen walieleza kusikitishwa na uamuzi huo lakini wakasema wanamheshimu na kumuunga mkono. Pia waliwahakikishia mashabiki wao kuwa wataendelea kutengeneza maudhui na kuendeleza miradi yao kama kawaida.

Kuondoka kwa KSI kunafunga ukurasa muhimu katika safari ya Sidemen, kundi ambalo limejikusanyia zaidi ya wafuasi milioni 140 duniani na kujitanua katika biashara za chakula, mavazi na matukio makubwa ya michezo.

Related Articles

Back to top button