Harmonize alalama wimbo wake kushushwa YouTube

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul maarufu Harmonize, amewasikitisha mashabiki wake baada ya kutangaza kuwa wimbo wake mpya wa Beautiful umeondolewa kwenye jukwaa la YouTube kutokana na madai ya ukiukwaji wa hakimiliki yaliyowasilishwa na mtu mwingine.
Kupitia taarifa rasmi aliyoitoa kwenye mitandao ya kijamii, Harmonize amesema tayari timu yake imeanza kufuatilia suala hilo ili kubaini chanzo cha tatizo na kuhakikisha haki inapatikana.
“Taarifa rasmi. Wapenzi mashabiki, tungependa kuwataarifu kuwa wimbo wetu mpya wa Harmonize uitwao Beautiful umeondolewa YouTube kutokana na dai la hakimiliki lililowasilishwa na mtu mwingine,” ameandika Harmonize.
Msanii huyo ameongeza kuwa timu yake inashughulikia suala hilo kwa karibu na kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kulitatua haraka.
“Timu yetu tayari inafuatilia suala hili kwa karibu na kuchukua hatua stahiki kulitatua.
Tunawaomba muwe na subira na muendelee kutuonesha upendo na uungwaji mkono wenu,” ameongeza.
Taarifa hiyo imeibua hisia mbalimbali kwa mashabiki wa Konde Gang, wengi wao wakionesha masikitiko yao kufuatia kuondolewa kwa wimbo huo ambao ulikuwa umeanza kupata mwitikio mzuri tangu ulipoachiwa.
Hadi sasa, Harmonize hajafafanua kwa kina kuhusu mmiliki wa dai hilo la hakimiliki wala chanzo halisi cha mgogoro huo, huku mashabiki wakisubiri majibu rasmi yatakayobainisha hatma ya wimbo huo.
Pamoja na changamoto hiyo, mashabiki wameendelea kumtia moyo msanii huyo na kuonesha imani kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi na wimbo wa Beautiful utarejea tena kwenye jukwaa hilo la video duniani.




