Nyumbani

Mngqithi ataja mbinu alizotumia kumuua Simba

DAR ES SALAAM:KOCHA wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema walivumilia presha ya Simba katika dakika za mwanzo wakiamini wapinzani wao wangekuja kufanya makosa, kabla ya kutumia nafasi hiyo kupata bao lililowapa ushindi wa Ngao ya Jamii.

Simba ilianza mchezo kwa kasi na kutawala sehemu ya mwanzo, lakini Yanga ilifanikiwa kuzuia presha hiyo bila kuruhusu bao, kabla ya Kangwanda kufunga kwa kichwa na kuipa timu yake ushindi wa 1-0.

“Tulijua wanaweza kuongeza presha, lakini kama tungeweza kuvumilia bila kufungwa, wangeanza kufanya mambo kwa pupa. Walifanya hivyo na tukapata nafasi nyuma ya safu yao ya ulinzi,” amesema.

Kocha huyo amesema kwa ujumla alifurahishwa na kiwango cha wachezaji wake, akieleza kuwa walionesha nidhamu ya kufuata mbinu, nguvu na hamu ya kupambana hadi mwisho.

“Kwa maoni yangu, tulitawala mchezo. Kulikuwa na nyakati za hatari katika dakika 10 za mwisho ambapo tulipoteza mipira kirahisi, lakini kwa ujumla vijana walifanya kazi kubwa. Najivunia juhudi zao, nguvu walizoweka na namna walivyofuata mbinu,” amesema.
Licha ya ushindi huo, Mngqithi amesema hataki kuuita ushindi huo kuwa mkubwa, bali ni ushindi mzuri kwao katika maandalizi ya msimu.

Mngqithi amewashukuru pia mashabiki wa Yanga kwa sapoti waliyoitoa uwanjani, akiwataka waendelee kujitokeza katika michezo ijayo.

“Ningependa kuona hali hii ya mashabiki katika michezo inayofuata, kwa sababu naamini wao ni mchezaji wetu wa 12 na watatusaidia kushinda michezo mingi ya soka,” amesema.

Related Articles

Back to top button