Mastaa

Wolper amjia juu Maimartha baada ya kumhusisha na Msomali

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Jaqueline Wolper, ameshindwa kuficha hisia zake na kumjibu mtangazaji na muundaji wa maudhui Maimartha Jesse baada ya kuchapisha video kwenye mitandao ya kijamii akimuhoji mfanyabiashara mmoja wa Kisomali huku akidai kuwa anahusishwa kimapenzi na Wolper.

Katika video hiyo, Maimartha alionekana akifanya mahojiano na mwanaume huyo huku akitoa madai yanayomhusisha na staa huyo wa filamu, jambo lililoibua mjadala miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Baada ya kuona video hiyo, Wolper aliingia kwenye sehemu ya maoni na kutoa onyo kali kwa Maimartha, akionyesha kutofurahishwa na maudhui yaliyokuwa yamechapishwa.

Kupitia ujumbe wake, Wolper alimtahadharisha Maimartha kuwa siku moja anaweza kukutana na mtu ambaye hatavumilia vitendo vya aina hiyo.

“Yaani wewe utakutana na mtu siku akupige kijini kichwa chini miguu juu, unakufa stendi watu wanajua unasubiri gari kumbe umekufa.

Sana wewe, mbona hujaweka voice yote,” ameandika Jaqueline Wolper.

Kauli hiyo imezua sintofahamu na mijadala tofauti mtandaoni, ambapo baadhi ya watu wameona Wolper alitoa majibu kutokana na kukerwa na madai hayo, huku wengine wakitaka wahusika hao kumaliza tofauti zao kwa njia ya maelewano.

Hadi sasa, Maimartha Jesse hajatoa majibu rasmi kuhusiana na kauli ya Wolper iliyovuta hisia za wengi kwenye mitandao ya kijamii.

Related Articles

Back to top button