ABC yamlaza Savio, Twalipo Queens yaitandika Mgulani

DAR ES SALAAM: ABC imepata ushindi wa pointi 68-65 dhidi ya Savio katika mchezo wa Ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Don Bosco, Upanga.
Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku timu hizo zikibadilishana uongozi katika robo mbalimbali kabla ya ABC kupata pointi muhimu katika robo ya mwisho na kuondoka na ushindi.
Savio ilianza vizuri kwa kuongoza robo ya kwanza kwa pointi 20-15, lakini ABC ikapunguza pengo katika robo ya pili na kufikia mapumziko ikiwa nyuma kwa pointi moja tu, 31-32.
Robo ya tatu iliendelea kuwa ya kusisimua, ABC ikigeuza matokeo na kuingia robo ya mwisho ikiwa mbele kwa pointi 48-47.
Katika robo ya nne, ABC ilidhibiti mchezo na kufikisha pointi 68, huku Savio ikimaliza ikiwa na pointi 65.
Katika mchezo mwingine, Twalipo Queens iliibuka na ushindi wa pointi 47-31 dhidi ya Mgulani Queens.
Mgulani Queens ilianza kwa kuongoza robo ya kwanza kwa pointi 11-10, lakini Twalipo Queens ilifanya mabadiliko makubwa katika robo ya pili na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa pointi 29-16.
Twalipo Queens iliendelea kuongeza tofauti katika robo ya tatu, ikiongoza kwa pointi 42-22, kabla ya kumaliza mchezo ikiwa na ushindi wa pointi 47-31.




