Ligi Ya Wanawake

Precious aaga Yanga Princess 

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa Yanga Princess, Precious Christopher, ameashiria kuondoka katika klabu hiyo baada ya kuandika ujumbe wa hisia wa kuaga.
Precious kupitia ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao, amesema Yanga Princess haikuwa klabu kwake pekee, bali ilikuwa kama nyumbani, huku akieleza kuwa licha ya ugumu wa kuondoka, atabeba kumbukumbu na yote aliyojifunza katika klabu hiyo kwa ajili ya maisha yake ya baadaye.
“Mwisho wa zama. Si klabu tu kwangu, imekuwa nyumbani. Ingawa ni vigumu kuondoka kwenye mlango huu, nabeba kila nilichopata hapa kwenda nacho katika maisha ya baadaye,” aliandika Precious.
Mchezaji huyo pia alitoa shukrani kwa uongozi wa klabu, makocha, wachezaji wenzake, mashabiki na wote waliomuamini katika kipindi chake akiwa Yanga Princess.
“Shukrani kwa bodi, makocha, wachezaji wenzangu, mashabiki na kila aliyeniamini. Mtakuwa na nafasi ya pekee moyoni mwangu,” ameandika.
Katika ujumbe wake huo, Precious alimalizia kwa kauli maarufu ya mashabiki wa Yanga, “Once Mwananchi, Always Mwananchi,” akisisitiza kuwa licha ya kuondoka, bado ataendelea kuwa sehemu ya familia ya Wananchi.

Related Articles

Back to top button