Zari ampongeza Princess Tiffah kufikisha miaka 11

MTOTO wa wasanii maarufu, Naseeb Abdul Juma maarufu kama Diamond Platnumz na Zarinah Hassan, Princess Tiffah, ametimiza umri wa miaka 11.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Zari alimpongeza binti yake huyo kwa kutimiza siku yake ya kuzaliwa, akieleza kuwa Princess Tiffah ni miongoni mwa watu wenye nafasi ya kipekee na umuhimu mkubwa katika maisha yake.
Tangu alipozaliwa, Princess Tiffah amekuwa akivutia umakini wa umma kutokana na umaarufu wa wazazi wake, huku pia akiwahi kuwa balozi wa kampuni mbalimbali zinazotoa bidhaa na huduma zinazohusiana na watoto.
Diamond Platnumz na Zari Hassan walijaliwa watoto wawili, Princess Tiffah na Prince Nillan, kabla ya kuhitimisha uhusiano wao.
Licha ya kutokuwa pamoja, wawili hao wameendelea kushirikiana katika malezi ya watoto wao na kushiriki pamoja katika matukio muhimu yanayowahusu.
Mara kadhaa, Zari husafiri na watoto kwenda Tanzania kumtembelea baba yao, huku Diamond naye akisafiri kwenda Afrika Kusini kuwaona watoto wake wanakoishi na mama yao.
Maadhimisho ya miaka 11 ya Princess Tiffah yamepokelewa kwa pongezi nyingi kutoka kwa mashabiki na watu mbalimbali waliomtakia afya njema, furaha na mafanikio katika hatua mpya ya maisha yake.




