Mitindo

Warembo 32 kuingia kambini Miss Universe 2026.

DAR ES SALAAM: Baada ya mchujo uliowahusisha zaidi ya warembo 100, jumla ya warembo 32 wamechaguliwa kuingia kambini kwa ajili ya mashindano ya Miss Universe Tanzania 2026.

Mchujo huo ulifanyika usiku wa kuamkia Agosti 3, katika Hoteli ya Ledger Plaza Bahari Beach jijini Dar es Salaam, ambapo washiriki waliofanikiwa wataanza kambi ya awali kwa kipindi cha wiki mbili kabla ya kufanyika mchujo mwingine utakaobakiza warembo 20 watakaoingia hatua ya Boot Camp.

Miongoni mwa waliofanikiwa kuingia kambini ni Miss Tanzania 2018, Queen Elizabeth Makune, pamoja na mshindi wa tatu wa Miss Tanzania 2018, Sandra Giovinazzo. Aidha, washiriki wengi waliochaguliwa ni nyuso mpya katika tasnia ya mashindano ya urembo.

Akizungumza baada ya mchujo huo, Mkurugenzi wa Miss Universe Tanzania, Happiness Magese, amesema maandalizi ya mwaka huu yanalenga kupata mshiriki mwenye uwezo wa kuiwakilisha Tanzania kimataifa na kushindana katika viwango vya juu.

Kwa upande wake, Miss Universe Tanzania 2025, Naisae Yona, amewataka washiriki kutumia kipindi cha kambi kujifunza, kujijengea uwezo na kujiandaa kwa ushindani uliopo mbele yao.

Baadhi ya washiriki waliozungumza baada ya kutangazwa kwa majina yao ni Irene Mbando, Miriam Ibrahim na Queen Elizabeth Makune, ambao wameeleza kufurahishwa na nafasi hiyo huku wakiahidi kufanya vizuri katika hatua zinazofuata za mashindano.

Related Articles

Back to top button